Vinara wa ligi kuu ya soka Tanzania bara (Wekundu Wa Msimbazi Simba) wameondoka jijini Dar es Salaam kuelekea Mtwara, tayari kwa mchezo wao wa kwanza wa mzunguko wa pili dhidi ya Ndanda FC.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya klabu hiyo, Hajji Sunday Manara ameiambia Dar24 kuwa, timu imeondoka na wachezaji 20 kwa ajili ya mchezo huo.

Simba watakuwa wageni wa Ndanda FC Jumapili kwenye uwanja wa Nangwanda Sijaona.

Hata hivyo Manara hakutaja wachezaji walioongozana na timu mjini humo, lakini Dar24 imebaini wachezaji ambao hawajakwenda kwa sababu mbalimbali ni Juuko Murshid, Mwinyi Kazimoto, Mussa Ndusha, Pastory Athanas, Emmanuel Semwanza na kipa Vincent Angban.

Muivory Coast Angban na Ndusha kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wanaachwa baada ya kusajiliwa wachezaji wapya kutoka Ghana, kipa Daniel Agyei na kiungo James Kotei.

Murshid bado yuko na timu yake ya taifa ya Uganda, Mwinyi Kazimoto ni majeruhi, Pastory Athanas hajakamilisha uhamisho wake kutoka Stand United na Emmanuel Semwanza ana matatizo ya kifamili.

Wachezaji waliotarajiwa kuwamo kwenye msafara huo ni makipa; Daniel Agyei, Peter Manyika, mabeki; Hamad Juma, Janvier Bokungu, Abdi Banda, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Novaty Lufunga na Method Mwanjali.

Viungo ni James Kotei, Jonas Mkude, Said Ndemla, Muzamil Yassin, Jamal Mnyate, Shizza Kichuya na washambuliaji Frederick Blagnon, Laudit Mavugo, Ame Ally na Ibrahim Hajib, Juma Luizio na Hajji Ugando.

Simba ilimaliza mzunguko wa kwanza wa ligi kuu ya soka Tanzania bara katika nafasi ya kwanza kwa pointi zake 35, mbili zaidi ya mabingwa watetezi, Young Africans.

Marekani yathibitisha Putin alisaidia kumpa ushindi Trump kupitia udukuzi
Picha: Fahamu kilicholipata jumba alilozaliwa Hitler