Mshike mshike wa ligi kuu ya soka Tanzania bara uliendelea tena hii leo kwenye uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera mjini Bukoba, ambapo mabingwa watetezi Wekundu Wa Msimbazi Simba walikua wageni wa wakata miwa kutoka Wilayani Missenyi, Kagera Sugar FC.

Mchezo huo uliokua unasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini kote kufuatia Simba kuwa na rekodi mbaya dhidi ya Kagera Sugar, kwa misimu miwili mfululizo, umeshuhudia dakika 90 zikishambuliwa vilivyo, huku kila upande ukihangaika kusaka alama tatu muhimu.

Hata hivyo mabavu, tambo na maneno kejeli vilivyokua vimetawala kabla ya matanange huo, vilimalizwa kwa wenyeji Kagera Sugar kumbilia kichapo cha mabao matatu kwa sifuri, yaliyofungwa na Meddie Kagere aliyefunga mawili, pamoja na beki wa pembeni na nahodha msaidizi Mohamed Hussein “Tshabalala”.

Kocha mkuu wa Kagera Sugar Meck Mexime aliwapongeza Simba mara baada ya mchezo huo, huku akisema wapinzani wao walitumia makosa walioyafanya kipindi cha kwanza na kufanikiwa kuufanya mchezo kuwa mwepesi kipindi cha pili, ambapo walipata bao la penati.

“Niwapongeze Simba kwa kucheza vizuri hii leo, walijipanga na walifanikiwa kutumia makosa yetu kipindi cha kwanza hadi wakapata mabao mawili ya kuongoza, na waliporudi kipindi cha pili mchezo ulikua rahisi sana kwao na wakafanikiwa kutufunga bao la tatu kwa penati.” Alisema Mexime

Naye kocha mkuu wa mabingwa wa Tanzania bara Simba SC Patrick Aussems, amewapongeza wachezaji wake kwa kazi nzuri waliyoifanya wakati wote wa dakika 90, huku akisisitiza kuufikia mchezo ujao dhidi ya Bishara United, utakaounguruma mjini Musoma, mkoani Mara mwishoni mwa juma.

“Sina budi kuwashukuru wachezaji wangu kwa kuonyesha mchezo mzuri, sasa tunaanza kujipanga kwa mchezo ujao dhidi ya Biashara United, tutakaoucheza siku ya jumapili.” Alisema Aussems.

Mchezo mwingine wa ligi kuu ya soka Tanzania bara uliochezwa leo, ulikuwa huko mkoani Iringa, kwenye uwanja wa Kumbukumbu ya Samora, ambapo imeshuhudiwa wenyeji Lipuli FC wakiwakabili Mbeya City kutoka mkoani Mbeya.

Matokeo ya mchezo huo, Lipuli FC wameshindwa kuunguruma nyumbani baada ya kulazimishwa sare ya mabao mawili kwa mawili.

Zanzibar chali cha ndege, yabanjuliwa 5-0
FC Barcelona yaadhibiwa Hispania