Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania – TANAPA, limeanzisha programu maalum ya watu wanaohitaji Majina yao yatumike kwa baadhi ya wanyama kulipia kiasi cha shilingi Milioni 5.
Akizungumza na Waandishi wa habari hii leo Julai 24, 2023 Jijini Dodoma Kamishna wa TANAPA, William Mwakilema amesema Programu hiyo imekuja kufuatia baadhi ya wanyama kupewa majina ya watu akiwemo Simba Bob Juniour, Faru aliyepewa jina la Faru John na Rajabu.
“Tumeanzisha program hiyo ya kuwapa majina yenu wanyama kama ilivyo kwa bob junior na baadhi ya wanyama wengine, hii program siyo bure mtalipia kiasi cha pesa na kama Mtu yoyote ambaye anataka aendelee kumuona mnyama aliyempa jina atatakiwa kuchangia gharama za kumuhifadhi shinilingi milioni 1 kila mwaka,” amesema Mwakilema.
Hata hivyo amesema bodi ya Menejimenti ya TANAPA imeshapitisha utaratibu huo ambao utaanza na wanyama aina ya faru na Simba Bob Juniour, alipewa jina hilo na waongoza utalii baada ya kumlinganisha mnyama huyo na Hayati Bob Marley aliyekuwa na rasta nyingi na ukubwa wa jina lile kuwa kivutio kwa watalii.