Mwandishi wa habari na mchambuzi wa Michezo nchini Gift Macha, amempa mbinu Mwekezaji wa Mabingwa Soka Tanzania Bara Mohamed Dewji ‘Mo’ ili kumaliza sintofahamu inayoendelea mitandaoni.
‘Mo’ amekua na wakati mgumu baada ya aliyekuwa Msemaji wa Simba SC Haji Manara kuzungumza na wanahabari mapema juma hili na kuweka wazi baadhi ya mambo aliyodai hayapo sawa klabuni hapo.
Guft ameandika kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii akimtaka ‘Mo’ kubadili muelekeo wa kujikita zaidi kwenye mitandao ya kijamii na kujibizana na wanaombeza.
Gift ameandika: “Haya ni mambo MATANO ya kurejesha heshima ya tajiri huyo inayoonekana kutetereka.
- Kuweka hadharani mipango yake ya muda mrefu Simba. Ipo haja sasa ya MO kueleza mipango yake ndani ya klabu hiyo. Inadaiwa kuwa fedha anazotoa kwa sasa ni kama mkopo, jambo ambalo linahitaji kutolewa ufafanuzi wa kina. Ni lazima MO aseme amepanga kuifanyia nini Simba na katika utaratibu upi?
- Kusaini mkataba wa Azam TV Katika kuonyesha kuwa Simba inaendeshwa kwa weledi, ni muda muafaka sasa kwa timu hiyo kusaini mkataba huo wa Azam TV… Kama ni kweli Simba walishakubaliana na Azam TV, ni wazi kuwa MO akiruhusu mkataba huu ukamilike, itampa heshima na kurejesha weledi ndani ya klabu.
- Kufafanua udhamini wa kampuni zake pale Simba… Baada ya kudaiwa kuwa jezi ya Simba ina matangazo kama ‘Timu za Sudan’, ipo haja ya MO kutoka hadharani na kuelezea undani wa mikataba hiyo na namna inainufaisha Simba.. Kwa sasa jezi ya Simba ina matangazo ya MO Xtra, MO Protector Sabuni, MO Foundation.. Na mengine ya vinywaji yanayowekwa kwenye kurasa rasmi za klabu.
- Kupunguza muda wake mitandaoni…. Kwa namna MO amekuwa akinyukana na watu MITANDAONI, ni vyema sasa akapunguza muda wake huko. Haileti picha nzuri kwa TAJIRI kunyukana na watu mitandaoni.
- Usajili wa maana …. Mwisho wa yote, Simba inatakiwa kufanya usajili mkubwa katika dirisha hili ili kurejesha heshima yake. Kama ni kweli Miquissone anaondoka, Simba inahitaji kushusha beki mpya wa Kati na straika wa maana zaidi. Usajili huu utaweka matumaini ya Simba kufanya vizuri zaidi katika michuano ya CAF.”