Rais wa Heshima wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Mohamed Dewji ‘Mo’ amesema klabu hiyo itaendelea kufanya usajili kwa kuiheshimu misingi na mikakati iliyojiwekea ili kuwa na kikosi imara.
Simba SC inahusishwa na taarifa za kuwafuatilia baadhi ya wachezaji wa Kimataifa kwa ajili ya msimu ujao huku Mshambuliaji wa Zanaco FC ya Zambia Moses Phiri na Victorien Adebayor wa USGN wakiongoza kutajwa katika taarifa hizo.
Akizungumza na Mashabiki na Wanachama wa Simba SC kupitia Mitandao ya kijamii leo Ijumaa (Machi 11) jioni, Mo Dewji amesema klabu ya Simba imekua na utaratibu wa kusajili kwa kuzingatia akili na kwa usiri mkubwa tangu ilipoingia katika mfumo mpya wa uwekezaji miaka minne iliyopita.
“Mambo ya usajili lazima yafanywe kwa akili kubwa na siri kubwa. Kwenye miaka hii minne tumejifunza mengi sana, naomba mtuamini kwamba hao wachezaji tunawafatilia kwa karibu kwa hiyo muda ukifika tutawambia.” Amesema Mo Dewji.
Kuhusu Mshambulaiji wa USGN Victorien Adebayor, Dewji amesema: “Ni mchezaji mzuri lakini yeye mwenyewe ana hamu ya kuja kucheza Simba, kwa hiyo kamati ya usajili wameshaanza kuongea nae na kama makubaliano yatafikiwa anaweza kucheza Simba msimu ujao.”
Simba SC imedhamiria kuendelea kukiboresha kikosi chake kwa msimu ujao wa Ligi Kuu na Michuano ya Kimataifa kama itapata nafasi hiyo, ili kuendelea kufanya vizuri kwenye Michuano ya ndani na nje ya Tanzania.