Raisi wa Heshima wa Klabu ya Simba Mohamed Dewji ‘Mo’ amewajibu baadhi ya wadau wa soka nchini wanalioibuka na kuhoji baadhi ya mambo kwenye mitandao ya kijamii, baada ya klabu hiyo kupoteza ubingwa wa Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ kwa kufungwa na Young Africans Jumamosi (Mei 28), katika uwanja wa CCM Kirumba.
Simba SC iliyokua inatetea ubingwa huo kwa mara ya tatu mfululizo ilikubali kupoteza mchezo huo kwa kufungwa 1-0, hali ambayo ilizua taharuki kwa baadhi ya wadau wa soka nchini ambao walihoji baadhi ya mambo ambayo wanahisi kuwa chanzo cha kuyumba kwa klabu hiyo msimu huu 2021-22.
Mapema leo Jumatatu (Mei 30) Mo ambaye pia ni Mwekezaji wa Simba SC, ametoa jibu kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, akionesha kusikia na kuona yaliyosemwa na kuandikwa katika mitandao hiyo baada ya mchezo wa juzi Jumamosi (Mei 28).
Mo ameandika: Kwa ujumla miaka 5 iliyopita imekuwa ya mafanikio kwa Simba. Bajeti iliongezeka mara 5, tulishinda makombe mengi ya ndani na tuliweka alama kimataifa kwa kufika robo fainali tatu za michuano ya Afrika.
Najivunia kuweza kusema tupo katika orodha ya vilabu bora 12 Afrika. Hii imekuwa mara ya kwanza Simba kuwa na mwendelezo mzuri katika miaka 86 ya historia yetu. Hakuna kurudi nyuma, tunatakiwa kufanya mabadiliko katika maeneo ambayo tuna madhaifu na kwenda mbele. Mapambano yanaendelea!