Mfanyabiashara maarufu nchini Mohamed Dewji, kwa mara ya kwanza ameongea kusimulia siku tisa za kutekwa kwake alipofanya mahojiano na shirika la utangazaji la Uingereza (BBC).

Amesema kuwa kwa siku zote hizo alipewa kipande cha khanga pekee kwaajili ya kujifunika na alilazimika kutii kila alichotakiwa kufanya kwa kuwa alihisi mwisho wa  maisha yake unakaribia.

” Saa 24 za kwanza baada ya kutekwa zilikuwa kama mwezi imani ndiyo kitu kikubwa kilichonisaidia kipindi kizima” ameeleza.

Amefafanua kuwa watekaji walimfunga macho, miguu na mikono kwa siku tisa “Asubuhi walikuwa wananifungua  mikono wananifunga mbele, lakini usiku, kulikuwa na mitihani walikuwa wananifunga nyuma, na wakikufunga nyuma maana yake huwezi kulala lazima ulalie kulia au kushoto”

Katika masimulizi ya jinsi tukio lilivyo tokea amesema ” Kufunga mlango wa gari tu, kugeuka nimekuta watu wanne ambao wamevaa mask nyeupe, wamefunika uso, wakapiga risasi juu mara mbili halafu wameniwekea bunduki”

Kwakuwa alidhani ni jaribio la kutaka kuibiwa gari, hakuwa na budi kufuata maagizo aliyopewa ya kulala sakafuni ambapo ndani ya sekunde 60 walimfuata na kumbeba.

Amesema walipoanza safari, watekaji walimvua nguo kwa kuhofia huenda anakifaa cha kutambua anakokwenda na wakamfunga mikono na miguu na dakika kama 20 wakamfikisha katika nyumba, wakiwa wanaongea lugha ya kigeni.

Ameeleza kuwa tokea Oktoba 11 alipo tekwa alikuwa akitoa ushirikiano kwa kila alichotakiwa kufanya huku akielekeza zaidi maombi kwa Mungu.

Baada ya siku tisa aliachiwa ” Waliinisukuma pale Gymkhana na nilisikia gari limeondoka” amesimulia

Baada ya kuachiwa kwake, kamanda wa Polisi wa kanda maalumu Dar es salam, Lazaro Mambosasa alisema watu waliomkamata walikuwa na lafudhi mojawapo ya lugha za mataifa ya kusini mwa Afrika.

Kuhusu uchunguzi ulipofikia Mo amesema hafuatilii uchunguzi huo ambao unaendelea kufanyika , ambao hadi sasa mtu mmoja anashtakiwa kuhusika na utekaji huo.

” Mimi ni mtu nasamehe watu, siweki vitu ndani ya moyo wangu” amesisitiza Mo Dewji.

Kwamujibu wa jarida la Forbes Mo Dewji mwenye umri wa miaka 43 ana utajiri wa dola 1.5 bilioni za Marekani.

Malalamiko uchaguzi serikali za mitaa yatua TAKUKURU
Video: Idriss Sultan yamkuta makubwa , 'Mnada wa wabunge wafungwa kwa uchafu'