Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Mohamed Dewji *Mo* amezika tofauti kati yake na Mbunge jimbo la Nzenga vijijini Khamis Kigwangala.

Wawili hao walijenga uhasama kupitia mitandao ya kijamii, kufuatia sakata la uwekezaji ndani ya klabu ya Simba SC, ambapo Kigwangala alianza kwa kuhoji uteuzi wa afisa mtendaji mkuu mpya Barbara Gonzalez miezi miwili iliyopita.

Baadae *Mo* alimjibu Mbunge huyo wa Jimbo la Nzenga vijijini ambaye pia ni mwanachama na shabiki wa klabu ya Simba, jambo ambalo lilizua taharuki na masuala mengine kujitokeza hadharani, huku wadau wengine wakichangia maoni *Comment*.

Mapema hii leo jumatano, Novemba 25 *Mo* ameandika kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii ujumbe ambao umedhihirisha kuzika tofauti zilizoibuka kati yake na Kigwangala.

“Nia njema ni tabibu, nia njema ni ibada. Sote tuna mapenzi ya dhati na Simba, hata tulipokwazana ilikua katika nia njema kwenye maendeleo ya timu yetu. Naomba radhi nilipokosea na mimi uliponikosea nishasamehe. Tuijenge Simba pamoja sasa. #NguvuMoja” ameandika Mo.

Hata hivyo ujumbe wa Mo, umekuja baada ya Kigwangala kuthibitisha kumaliza tofauti zilizokuwepo kati yao siku nne zilizopita, ambapo naye aliandika kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.

“Wanasimba tunataka ushindi dakika 90 uwanjani na mchango wa Mohammed siyo wa kudharau kwenye hili, lakini hata yeye na biashara zake wanafaidika na Simba as a brand, siyo bure tu.”

Thamani ya Simba siyo majengo, ni brand yenye umri wa zaidi ya miaka 80. Tanzania ni lazima uwe Simba ama wale wengine…hata kama unamiliki timu yako. Siyo kitu kidogo.

“Simba ina maslahi ya umma. Ninaweza kusema mengi lakini siyo lengo langu. Nimekuwa nikiwaza juu ya kusameheana. Yaishe. Tusonge mbele. Naomba radhi kwake na kwa washabiki wote wa Simba niliowakwaza. Mimi nimesamehe. Maisha yaendelee. #HK #NguvuMoja” sehemu ya ujumbe wa alioandika Kingwangala kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Halima Mdee na wenzake kikaangoni CHADEMA
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Novemba 25, 2020