Rais wa Heshima wa Klabu ya Simba, Mohamed Dewji ‘Mo’ leo Ijumaa (April 21) amepanga kukutana na wachezaji wa timu hiyo pamoja na benchi la ufundi kwa ajili ya kuwapa hamasa kuelekea mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Robo Fainali wa michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Wydad Casablanca, utakaopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.
Meneja wa Habari wa klabu hiyo, Ahmed Ally ameeleza kuwa lengo la Mo ni kuwaongezea hamasa wachezaji wao na kuwapa motisha ili wapambane na kupata ushindi mnono utakaowaweka kwenye mazingira mazuri ya kusonga mbele.
“Ni kawaida ya Mo kuzungumza na wachezaji kila tunapokabiliwa na mchezo wa kimataifa kama huu, ni hamasa nzuri kwa wachezaji wetu kutokana na ahadi ambazo wanapewa na kiongozi huyo mwenye mapenzi ya dhati na Simba,” amesema Ahmed.
Meneja huyo ameeleza kuwa katika hafla hiyo, Mo ataambatana na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Salim Abdallah ‘Try Again’ pamoja na Mwenyekiti wa klabu hiyo, Murtaza Mangungu.
Ahmed amesema maandalizi ya timu yao kuelekea mchezo huo wa kesho ambao unatarajiwa kuanza saa 10 jioni yanakwenda vizuri na wachezaji wao wapo tayari kwa ajili ya kuikabili miamba hiyo ya Afrika, Wydad Casablanca ambao ni mabingwa watetezi.
Amesema wanakwenda kwenye mchezo huo wakiwa na imani kubwa na wachezaji wao kutokana na kazi waliyoifanya huko nyuma hadi kufika hatua hiyo waliyopo hivi sasa ya Robo Fainali.
“Wachezaji wetu pamoja na benchi la ufundi wamefanya kazi kubwa, wametufikisha robo fainali michuano ya Afrika lakini pia wamefanya kazi kubwa ya kumfunga mtani wetu Young Africans wiki iliyopita, sasa kazi iliyopo mbele yao ni kutupeleka Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika,” amesema Ahmed.
Katika mchezo huo Simba SC italazimika kupata ushindi mnono wa kuanzia mabao matatu kwenda mbele ili kuweka ugumu katika mechi ya marudiano ambayo itapigwa nchini Morocco Aprili 29.