Mashabiki na Wanachama wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC wameombwa kujitokeza Uwanja wa Benjamin Mkapa siku ya Jumapili (Machi 13) kwa idadi kamili, iliyoruhusiwa na Shirikisho la soka Barani Afrika ‘CAF’.
Simba SC itacheza dhidi ya RS Berkane katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika, huku ikiwana lengo la kusaka ushindi utakaoiweka kwenye nafasi nzuri ya kufuzu hatua ya Robo Fainali ya Michuano hiyo.
Wito kwa Mashabiki na Wanachama wa Simba SC umetolewa na Rais wa Heshima Mohamed Dewji ‘Mo’ alipozungumza na moja kwa moja na Wanasimba kupitia mitandao ya kijamii leo Ijumaa (Machi 11) jioni.
Dewji amesema Mashabiki na Wanachama wa Simba SC wanapaswa kufika uwanjani kwa idadi iliyorusiwa ili kufanikisha azma ya kuwawezesha wachezaji wao kucheza kwa ari kubwa, ili kutimiza lengo la ushindi unaotakiwa.
“Wapinzani wetu lazima wajue wapo away, kwanza inawatisha. Mimi nikija uwanjani siwezi kukaa, nasimama napiga kelele, inatoa ari kubwa kwa wachezaji kujitoa zaidi. Naomba mashabiki wote 35,000 tujitokeze, asipungue hata mmoja.” Amesema Mo Dewji
Kuhusu mpango wa Mashabiki wa Simba SC kuimba wimbo maalum wa kwa pamoja ili kuwapa hamasa wachezaji watakapokua na kazi ya kuikabili RS Berakane Jumapili (Machi 13), Mo Dewji amesema mpango huo ulikuwa sehemu ya ndoto zake na anashukuru kuona umetambulishwa rasmi kupitia Idara ya Habari na Mawasilino.
“Hiyo ilikuwa ndoto yangu, sisi tuimbe kwa pamoja, tuimbe nyimbo moja. Nikupongeze wewe (Meneja wa Habari na Mawasiliano) kwa kazi nzuri.” Amesema Mo Dewji
Simba SC ilipoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya RS Berkane katika mchezo wa Mzunguuko wa tatu wa Kundi D, Februari 27 mjini Berkane-Morocco hivyo itahitaji kulipa kisasi kwa kusaka ushindi ili kurejea kileleni mwa msimamo wa Kundi hilo.
Kabla ya mchezo huo Simba SC ilikua inaongoza msimamo wa Kundi D kwa kuwa na alama 04, huku Berkane iliyopoteza mchezo wa Mzunguuko wa pili dhidi ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast ilikua na alama 03.
Hadi sasa Msimamo wa Kundi D, unaonyesha kuwa RS Berkane inaongoza ikiwa na alama 06, ikifuatiwa na Simba SC yenye alama o4 sawa na USGN ya Niger huku ASEC Mimosas ya Ivory Coast ikiburuza mkia ikiwa na alama 03.