Rais wa Heshima na Mwekezaji mwenza wa Klabu ya Simba SC Mohamed Dewji ‘Mo’ amesisitiza kutokurudi nyuma baada ya kutinga hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu huu 2022/23.
Simba SC jana Jumapili (Oktoba 16) ilitinga Hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kwa kuichapa CD Primeiro de Agosto ya Angola bao 1-0, baada ya kufanya, hivyo ugenini kwa ushindi wa 1-3.
Mo ametumia kurasa zake za Mitandao ya Kijamii akionyesha furaha ya kuiona Simba SC ikitinga Hatua ya Makundi kwa mara ya tatu ndani ya miaka mitano upande wa Ligi ya Mabingwa na mara moja Kombe la Shirikisho.
Mo aneandika: “Familia yangu ya Simba. Mwanzoni mwa msimu wa ligi, niliandika hivi: Kwa ujumla miaka 5 iliyopita imekuwa ya mafanikio kwa Simba. Bajeti iliongezeka mara 5, tulishinda makombe mengi ya ndani na tuliweka alama kimataifa kwa kufika robo fainali tatu za michuano ya Afrika.”
“Najivunia kuweza kusema tupo katika orodha ya vilabu bora 12 Afrika. Hii imekuwa mara ya kwanza Simba kuwa na mwendelezo mzuri katika miaka 86 ya historia yetu.”
“Hakuna kurudi nyuma, tunatakiwa kufanya mabadiliko katika maeneo ambayo tuna madhaifu na kwenda mbele. Mapambano yanaendelea! ?? #nguvumoja”