Kocha Mkuu wa KMC FC, Abdulhimid Moallin amezitabiria makubwa timu za Simba SC na Young Africans katika mechi za mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kutokana na ubora wa vikosi walivyokuwa navyo.
Akizungumza jijini Dar es salaam kocha huyo aliyewahi kuinoa Azam FC msimu uliopita, amesema timu hizo mbili zimeimarika sana na kama viongozi pamoja na wachezaji watakuwa makini zinaweza kufika hatua za mwisho ikiwemo kubeba ubingwa wa taji hilo la Afrika.
“Navutiwa sana na ushindani wa Simba SC na Young Africans hasa mtazamo wao wa kutaka kufanya vizuri kwenye mashindano ya CAF, zimeonesha dhamira ya kweli kuanzia kwenye usajili wao na jinsi wanavyocheza, ukweli kama wataendelea hivyo nawaona mbali sana,” amesema Moallin.
Kocha huyo amesema msimu huu tayari amekutana na Young Africans kwenye Ligi Kuu na kipigo cha mabao matano alichopewa kilidhihirisha ukubwa na ubora wa timu hiyo na maandalizi yao kuelekea mechi hizo.
Akizungumzia timu yake ya KMC, kocha huyo amesema wameendelea kuimarika kwa kujenga muunganiko wa wachezaji huku akiamini mapumziko ya majuma mawili waliyoyapata yamemsaidia kukamilisha vitu ambavyo hawakuwa navyo wakati msimu mpya unaanza.
Amesema pamoja na ushindani uliopo kutoka kwa timu za Simba SC, Young Africans na Azam FC lakini anaamini nafasi ya kufanya vizuri na kumaliza ligi kwenye nafasi za juu ni kubwa kwao kutokana na aina ya wachezaji waliowasajili kwenye kikosi chake.
KMC ambayo msimu uliopita ilinusurika kushuka daraja inashika nafasi ya 15 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu ikiwa na pointi moja katika mechi mbili ilizocheza hadi sasa.