Kiungo wa Real Madrid na timu ya taifa ya Croatia, Luka Modric ameshinda tuzo ya Ballon d’Or kwa mwaka 2018, na kuwa mchezaji wa kwanza tofauti na Lionel Messi na Cristiano Ronaldo kushinda tuzo hiyo baada ya miaka 10.

Modric, 33, ameshinda kombe la Klabu Bingwa Ulaya mwezi Mei kwa mara ya tatu mfululizo na kulisaidia taifa lake kufika hatua ya fainali katika michuano ya Kombe la Dunia.

Mchezaji wa zamani wa Brazil na AC Milan Kaka, alishinda tuzo hiyo mwaka 2007, na baada ya hapo Messi na Ronaldo wameshinda mara tano kila mmoja tuzo hiyo ya thamani kwa wachezaji wa kandanda duniani.

Aidha, Ronaldo ambaye amehamia Juventus msimu huu amemaliza katika nafasi ya pili mwaka, huku Messi akishika nafasi ya tano. nafasi ya tatu ameshika mshambuliaji wa Atletico Madrid, Antoine Griezmann huku mshambuliaji wa PSG Kylian Mbappe akishika nafasi ya nne.

“Huu umekuwa ni mwaka wa kipekee sana kwangu, ni vigumu kuzielezea hisia zangu kwa maneno. Ni kitu cha pekee sana kwangu.”amesema Modric

Hata hivyo, tuzo ya Ballon d’Or imekuwa ikitolewa nchini Ufaransa kila mwaka toka 1956, na mshindi wake wa kwanza alikuwa mchezaji kutoka Uingereza Stanley Matthews.

Makala: Ni ipi nguvu halisi ya Bernard Membe CCM?
Majaliwa awafunda wakuu wa mikoa