Beki wa kushoto na Nahodha Msaidizi wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, amesema timu yao imedhamiria kufuzu harua ya Robo Fainali, Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
‘Tshabalala’ ametoa kauli hiyo kabla ya Simba SC haijaondoka Dar es salaam leo Ijumaa (Machi 18) alfajiri kuelekea nchini Benin, tayari kwa mchezo wa Mzunguuko watano wa Kundi D, dhidi ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast utakaopigwa Jumapili (Machi 20).
Beki huyo amesema wachezaji wote wamedhamiria kuifikisha Simba SC hatua ya Robo Fainali, kisha wataangalia uwezekano wa kuifikisha Nusu Fainali na hata Fainali.
“Dhamira yetu ni kwenda hatua kwa hatua, kwa sasa tupo hatua ya Makundi, tukifuzu tunakwenda Robo Fainali, hivyo kila hatua ina wakati wake, kwa sasa tunajipanga ili kuivusha Simba SC katika hatua hii,”
“Kufika Fainali inawezekana lakini huwezi kufika huko kama hujapita katika hatua nyingine, kila mmoja wetu anataka kucheza Fainali, lakini tuangalie kwanza umuhimu wa hatua tuliopo kabla ya kuanza kufikiria kucheza Fainali ya Michuano hii.”
“Tunashukuru kwa nafasi ambayo tupo kwenye msimamo, tumesaliwa na michezo miwili muhimu ambapo tunahitaji kuhakikisha tunapata matokeo mazuri ili kufuzu hatua ya Robo Fainali.”
“Tunaamini katika ubora ambao kikosi chetu kinaendelea kuuonyesha katika michuano hii, ni wazi kama tutafanikiwa kufuzu Robo Fainali, basi uzoefu tulioupata msimu uliopita kwenye hatua hiyo utatusaidia.” amesema ‘Tshabalala’
Simba SC inaongoza msimamo wa Kundi D ikiwa na alama 07 baada ya kuifunga RS Berkane Jumapili (Machi 13), Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es salaam, huku ASEC Mimosas ikiwa nafasi ya pili kwa ufikisha alama 06.
RS Berkane imefungana kwa alama na ASEC Mimosas lakini ipo nafasi ya tatu, huku USGN ikiburuza mkia wa Kundi D kwa kufikisha alama 04.