Imethibika kuwa Beki kutoka Ivory Coast Mohamed Ouattara ameutaka Uongozi wa Simba SC kuvunja mkataba wake ili aweze kuondoka na kwenda kujiunga na klabu nyingine.
Beki huyo kutoka nchini Ivory Coast alisajiliwa Simba SC akitokea Al Hilal ya Sudan mwanzoni mwa msimu huu, akisaini mkataba wa miaka miwili.
Mmoja wa Mabosi wa Simba SC amefichua kinachoendelea baina ya Beki huyo na Uongozi wa klabu hiyo ya Msimbazi kwa kusema, Ouattara ameomba mkataba wake uvunjwe ili katika Dirisha Dogo la Usajili aondoke.
Bosi huyo amesema sababu kubwa ya Beki huyo kutaka kuondoka wakati wa Dirisha Dogo la Usajili ni baada ya kukosa nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza chini ya Kaimu Kocha Mkuu Juma Mgunda.
“Ouattara ana wakati mgumu sana kuendelea kubaki Simba SC, anaendelea kuzungumza na viongozi ili mkataba wake uvunjwe kabla ya Dirisha Dogo la Usajili halijafunguliwa mwezi Januari 2023,”
“Shinikizo la kushindwa kucheza kwenye kikosi cha kwanza chini ya Kocha Mgunda limekua sababu kubwa sana kwake kutaka mkataba wake uvunjwe, anahitaji kwenda mahala pengine ambapo ana imani ataweza kucheza mara kwa mara.” amesema Bosi huyo
Ouattara wakati Simba SC kikiwa chini ya Kocha Mkuu Zoran Maki alikua akipata nafasi kucheza kwenye kikosi cha kwanza, huku Beki kutoka nchini Kenya Joash Onyango akisota Benchi.
Kwa sasa hali imekua tofauti, kwani Joash Onyango amekua chaguo la kwanza na Ouattara anasubiri Benchi.