Mshambuliaji wa klabu ya Liverpool Mohamed Salah, ameonekana katika fukwe za nchi ya Panama akiponda raha, baada ya kukamilisha jukumu la kuiwakilisha nchi yake ya Misri, kwenye fainali za kombe la dunia zilizofikia tamati mwishoni mwa juma lililopita.
Salah ameonekana katika fukwe za nchi hiyo ya Amerika ya kati akiwa pekee yake, na kwa sasa anatumia muda wa kuponda raha kufuatia mapumziko aliyopewa na uongozi wa klabu ya Liverpool kabla ya kurejea England kuendelea na maandalizi ya msimu mpya wa ligi.
Mpaka sasa haijafahamika kama mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 26 ameongozana na familia yake kwa ajili ya mapumziko hayo, japo ni kawaida kwa wachezaji kuwa na familia zao wanapokua mapumzikoni.
Hata hivyo imeshathibitika Salah hatokua sehemu ya kikosi cha Liverpool kitakachocheza michezo ya awali ya ligi ya nchini England, kutokana na madaktari kushauri apumzike ili apate nafasi ya kupona vyema jeraha la bega, alilolipata wakati wa mchezo wa fainali ya ligi ya mabingwa barani Ulaya dhidi ya Real Madrid uliochezwa Mei 26 mjini Kiev-Ukraine.
Pamoja na kuonekana akiwa na timu yake ya taifa ya Misri, bado Salah alihitaji muda wa kupumzika licha ya kucheza michezo ya kombe la dunia dhidi ya Urusi na Saudi Arabia.
Wakati akiponda raha huko Panama, mshambuliaji huyo tayari ameshasaini mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia Liverpool mapema mwezi huu, ambao utamuwezesha kulipwa mshahara wa Pauni 200,000 kwa juma.
Msimu wa 2017/18, Salah alikua na kiwango kizuri cha kusakata soka, ambacho kilimpelekea kufunga mabao 44 akiwa na Liverpool.