Mshambuliaji kutoka nchini Misri na klabu ya Liverpool Mohamed Salah Ghaly, ametangazwa kuwa mshindi wa tuzo ya mchezaji bora ya chama waandishi wa habari za michezo nchini Engalnd kwa msimu wa 2017/18 (FWA Player of the Year).
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 25, amekua na msimu mzuri, huku akiifungia klabu yake mabao 43 katika michezo yote aliocheza, sambamba na kuiongoza timu yake katika ushindi wa mabao matano kwa mawili dhidi ya AS Roma juma lililopita katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa nusu fainali, ligi ya mabingwa barani Ulaya.
Hatua ya kufikisha mabao 43, imemfanya mshambuliaji huyo kutoka barani Afrika kuivunja rekodi iliyowahi kuwekwa na washambuliaji waliocheza katika ligi ya England Alan Shearer, Cristiano Ronaldo na Luis Suarez – ambao kila mmoja alifunga mabao 31 kwa wakati wake.
Chama cha waandishi wa habari za michezo nchini England (FWA), kimetoa sababu ya kumtunuku Salah tuzo ya msimu huu, kwa kusema uwezo na ujasiri aliouonyesha akiwa na Liverpool umewapa msukumo wa kufanya hivyo.
Juma lililopita Salah alitangazwa kushinda tuzo ya mchezaji bora wa chama cha wachezaji wa kulipwa nchini England (PFA), hivyo tuzo ya FWA inakua ya pili kwake kwa msimu huu.
Liverpool ilimsajili Mohamed Salah mwanzoni mwa msimu huu kwa ada ya Pauni milioni 35, akitokea AS Roma ya Italia, na amekua na mahusiano mazuri kimchezo na washambuliaji wenzake klabuni hapo Sadio Mane na Roberto Firmino.