Mshambuliaji kutoka nchini Misri na klabu ya Liverpool Mohamed Salah, ana matumaini makubwa ya kuwakabili Manchester United, kufuatia taarifa za jeraha lake kuleta ahuweni kwa mashabiki.

Salah aliumia jumamosi, wakati wa mchezo dhidi ya Leicester City, baada ya kuchezewa rafu na kiungo Hamza Choudhury, kitu ambacho kiliwashtua mashabiki wa Liverpool ambao wanahitaji kumuona akiendelea kuzichachafya ngome za timu pinzani msimu huu.

Majibu ya vipimo alivyofanyiwa mshambuliaji huyo, yameeleza kuwa hakuumia sana kama ilivyofikiriwa, na kwamba aliteguka kifundo cha mguu kwa kiasi kidogo.

Hata hivyo mpaka sasa haijatangazwa ni lini Salah atarejea uwanjani, ila kinachoelezwa ni kwamba hatakuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu, na huenda akawa sehemu ya kikosi kitakachoikabili Manchester United.

Choudhury alionyeshwa kadi ya njano kutokana na rafu aliyomchezea Salah, huku meneja wa Liverpool Jurgen Klopp akiamini kwamba lilikuwa ni tukio ambalo lilipaswa mchezaji huyo kupewa adhabu kali zaidi.

“Rafu za aina kama ile kwangu mimi, sitaki kumzungumzia huyo mchezaji tena, ila ilipaswa kuwa kadi nyekundu,” alisema Klopp.

“Ilikuwa hatari sana. Kuna hatari nyingi, lakini hii ni moja ya hatari hizo. Sio kwamba nilitaka mchezaji atolewe kwa kadi nyekundu, la isipokuwa yalikuwa makosa ya makusudi yaliyolenga kuumiza.”

Baada ya kupisha michezo ya kimataifa, majogoo wa jiji “Liverpool” watakua wageni wa Manchester United huko Old Trafford, Oktoba 20.

 

Mpango wa Gerard Pique washtukiwa
Ukandamizaji kabila la Uighurs: Marekani yafungia makampuni 28 ya China