Mshambuliaji kutoka nchini Misri Mohamed Salah amesema ana matumaini ya kucheza fainali za kombe la dunia, licha ya kukabiliwa na jeraha ya bega, alilolipata wakati wa mchezo wa hatua ya fainali wa ligi ya mabingwa barani Ulaya usiku wa jumamosi dhidi Real Madrid.

Matumaini ya kushiriki fainali hizo kwa Salah, yamedhihirika kufuatia ujumbe waliouandika katika ukurasa wake wa Tweeter ili kuwatoa hofu mashabiki wake, ambao waliingia simanzi baada ya kuona tukio la kuumia.

“Ulikua usiku mgumu, lakini mimi ni mpambanaji, nina matumaini ya kuwa sehemu ya kikosi cha Misri kitakachokwenda nchini Urusi, ili kuwafanya muwe na cha kujivunia. Mapenzi na ushirikiano wenu utanipa nguvu ninazozihitaji.” Ameandika Salah.

Salah mwenye umri wa miaka 25, alilazimika kutoka uwanjani na nafasi yake kuchukuliwa na Adam Lallana dakika ya 30 kipindi cha kwanza, baada ya kupata majeraha hayo yaliyosababishwa na beki na nahodha wa Real Madrid Sergio Ramos.

Mshambuliaji huyo aliondoka uwanjani usiku huo, mara baada ya mchezo kumalizika kwa klabu yake kufungwa mabao matatu kwa moja, akiwa amevalishwa kitambaa kilichobeba mkono wake wa kushoto na kuzunguushiwa shingoni, kutokana na maumivu makali yaliyokua yakimkabili.

Salah alikua akipewa nafasi kubwa ya kuisaidia Liverpool katika mchezo huo, lakini kutoka kwake nje ya uwanja kulionyesha dhahir, majogoo wa jiji walikua na nafasi ndogo ya kuishinda Real Madrid, jambo ambalo lilitokea baadae.

Salah alikua muhimili mkubwa katika kikosi cha Liverpool tangu mwanzoni mwa msimu huu, na aliiwezesha klabu hiyo kufika hatua ya fainali ya ligi ya mabingwa barani Ulaya, kwa kushirikiana vyema na wachezaji wengine.

Video: Lissu kufanyiwa upasuaji wa mwisho Juni 4, CCM yakanusha katibu wake Kinana kujiuzulu
James Tarkowski aondolewa kambini St George's Park