Mshambuliaji wa majogoo wa jiji Liverpool Mohamed Salah Ghaly, amewataka mashabiki wa soka duniani, kutomshindanisha na Cristiano Ronaldo, kuelekea mchezo wa fainali wa ligi ya mabingwa barani Ulaya.
Liverpool ilifanikiwa kukata tiketi ya kucheza fainali ya ligi ya mabingwa barani Ulaya usiku wa kuamkia leo, licha ya kufungwa mabao manne kwa mawili dhidi ya AS Roma, na kuifuata Real Madrid ambayo ilitangulia kwenye mchezo huo kwa kuifunga FC Bayern Munich.
Salah, ambaye amefunga mabao 43 katika michuano yote aliocheza msimu huu, amesema mchezo wa fainali utakua kati ya Liverpool na Real Madrid na hauwezi kuwa kati yake na Cristiano Ronaldo.
Amesema anafahamu wakati wowote mijadala itaanza kuibuliwa katika mitandao ya kijamii kuhusu uwezo aliouonyesha msimu huu na kuchangia kuifikisha Liverpool katika mafanikio ya kucheza mchezo huo, dhidi ya mshambuliaji huyo wa Real Madrid.
“Mchezo wa fanali hauwezi kuwa wa wachezaji wawili pekee, bali utakua dhidi ya timu mbili zilizofanikiwa kucheza hatua hiyo, sitofurahia kuona mijadala ikiibuka kunihusu mimi na Ronaldo,” Amesema Salah.
“Ni kweli kwa sasa ninacheza katika klabu kubwa na yenye wachezaji wakubwa duniani, hivyo kufaulu kucheza fainali kumetokana na juhudi zetu sote na sio uwezo wa mchezaji mmoja mmoja, hivyo sipaswi kushindanishwa na yoyote.
“Suala la kufunga mabao ni sehemu ya kazi yangu, lakini bado mchezaji mwingine yoyote anaweza kufunga kutokana na nafasi inayopatikana uwanjani, kwa hiyo Liverpool ni ya wote na sio ya Salah pekee yake.”
Liverpool imesonga mbele katika michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya kwa ushindi wa jumla wa mabao 7-6 dhidi ya AS Roma, ili hali Real Madrid wameivurumisha FC Bayern Munich kwa jumla ya mabao 4-3.
Mchezo wa fainali kwa wawili hao utachezwa Mei 26 mjini Kiev nchini Ukraine.