Kikao cha Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF ilikutana Jumamosi Februari 10, 2018 kupitia mashauri yaliyofikishwa kwenye kamati hiyo.
Shauri namba moja lilihusisha malalamiko dhidi ya wachezaji Saba(7) wa timu ya Transit Camp,shauri ambalo lilihudhuriwa na mchezaji mmoja Mohamed Suleiman Ussi.
Mchezaji Mohamed Suleiman Ussi alituhumiwa kwa kosa la utovu wa nidhamu kwenye mechi namba 48 ya Kundi C Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara akidaiwa kutaka kumpiga Mwamuzi wa mchezo kinyume na Ibara ya 50(1)(2) na (5)ya Katiba ya TFF toleo la 2015.
Kamati ilipitia ripoti ya kamishna wa mechi ambayo pamoja na kuwataja wachezaji wengine wengine pia ilimtaja Mohamned Suleiman Ussi kuhusika kwenye tukio hilo akiwa amevaa jezi namba 14 ambaye pia alitajwa kwenye ripoti ya mwamuzi ikielezea kitendo cha Mohamed Suleiman Ussi kutaka kumpiga mwamuzi msaidizi namba 2.
Baada ya kupitia ripoti Kamati imejiridhisha kuwa mchezaji Mohamed Suleiman Ussi alitaka kumpiga mwamuzi kinyume na kanuni ya 36 ya Ligi Daraja la Kwanza na ibara ya 50(1)(2) na (5) ya Katiba ya TFF toleo la 2015.
Kamati imemuadhibu Mohamed Suleiman Ussi imemfungia kutocheza michezo mitatu(3) pamoja na faini ya Shilingi laki tatu(300,000) kwa mujibu wa kanuni ya 37(7) na 37(12) kanuni za Ligi Daraja la Kwanza.