Beki kutoka nchini Ivory Coast Mohammed Ouattara wakati wowote kuanzia sasa atatangazwa kuondoka Simba SC, baada ya kumalizana na Uongozi wa Klabu hiyo.
Taarifa kutoka Msimbazi zinaeleza kuwa, Beki huyo alikutana na Uongozi wa Simba SC na kufikia makubaliano ya kuvunjwa kwa mkataba wake, kufuatia kushindwa kuingia katika kikosi cha kwanza tangu aliposajiliwa mwanzoni mwa msimu huu 2022/23, chini ya utawala wa Kocha Mkuu Zonarn Maki.
Outtara alisajiliwa Simba SC akitokea Al Hilal ya nchini Sudan akisaini mkataba wa miaka miwili, na moja kwa moja alijiunga na kikosi cha klabu hiyo nchini Misri kilipokuwa kimeweka kambi ya kuajiandaa na msimu.
Taarifa zinaeleza kuwa Ouattara amekubali kuondoka Simba SC kwa makubaliano ya pande zote mbili kufikia muafaka, na tayari uongozi umeanza mazungumzo na baadhi ya mabeki wa kati watakaokuja kuchukua nafasi yake na kucheza pamoja na Mkongomani, Hennock Inonga.
“Mazungumzo ya pande zote mbili baina ya beki Ouattara na Uongozi wa Simba SC yamefikia katika sehemu nzuri ya yeye kuondoka hapo baada yeye mwenyewe kuridhia.
“Wakati wowote Ouattara anatarajiwa kupanda ndege kurejea nyumbani kwao huku akiweka mikakati ya kwenda kutafuta changamoto sehemu nyingine.
“Ouattara hakuwa na msimu mzuri tangu ajiunge na Simba SC baada ya majeraha kumuandama mara kwa mara huku akipoteza nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza,” zimeeleza taarifa kutoka kwa mmoja wa viongozi ndani ya Bodi ya Wakurugenzi
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally amezungumzia hilo kwa kusema: “Kila kitu kinachohusiana na usajili kwa hivi sasa kipo kwa kocha wetu Robertinho (Roberto Oliveira), na hivi karibuni kitawekwa wazi kila kitu baada ya taratibu kukamilika za kusajili na kuacha wale wachezaji wanaotakiwa kuachwa.”