Kiongozi wa chama cha upinzani cha Narc-Kenya, Martha Karua ameeleza kuwa Rais wa zamani wa Taifa hilo, Hayati Daniel Arap Moi alikuwa na sura mbili wakati wa utawala wake.
Akizungumza jana katika mahojiano na Citizen TV, Karua ameeleza kuwa Moi alikuwa na sura mbili, moja ya kiongozi mwenye ‘mkono wa chuma’ lakini unapokutana naye uso kwa macho alikuwa tofauti.
“Alikuwa na sura mbili, sura ya kiongozi aliyetawala kwa kutumia mkono wa chuma, lakini ukikutana naye uso kwa uso alikuwa mtu tofauti kabisa; alikuwa mjamii sana,” alisema Karua.
Mwanasiasa huyo alisimulia tukio analolikumbuka la mwaka 2001, alipoamua kutoka kwenye meza kuu akiwa amekaa karibu na Rais Moi, na kuondoka kwenye mkutano huo wa Rais baada ya kutokubaliana na kilichokuwa kinasemwa na wafuasi wake dhidi ya upinzani.
Karua ambaye wakati huo alikuwa Mbunge wa Gichugu, alieleza kuwa anakumbuka ilikuwa Juni 16, 2001, ambapo baadhi ya viongozi wa chama cha KANU cha Moi walikuwa wanazungumza wakidai ni bora Moi aachiwe awe Rais kwa kipindi chote cha maisha yake.
Wengine walishambulia upande wa upinzani wakidai kuwa wapinzani hawajui thamani ya uhuru wa nchi hiyo.
Alisema kuwa yeye aliamua kumsogelea Moi akiwa amekaa kiti kilichofuata na kumuomba awakataze wafuasi wake kutoa kauli hizo au amruhusu yeye azungumze ili kuweka mambo sawa, na baada ya kukataliwa aliona ni bora aondoke.
“Nilikuwa nimekaa karibu naye, nilimuomba anisikilize, alinisikiliza, nilimwambia naomba anipe nafasi nizungumze ili niweke mambo sawa kwa sababu yaliyokuwa yanasemwa na watu wake sio sahihi. Alinikatalia lakini alinihakikishia kuwa ‘yeye asingesema hayo yanayosemwa na watu wake’. Lakini hakuwakataza, na hakunipa nafasi ya kuzungumza,” Karua alisimulia.
Anasema yeye anaamini kuwa anaamini kama kiongozi hakemei kinachofanywa na wanajeshi wake wa mguu, basi ni sawa na kubariki wanachofanya. Hivyo, aliamua kusimama na kuondoka bila woga, lakini hakuzuiwa au kusumbuliwa.
Akizungumzia kitu kizuri zaidi anachokikumbuka kufanywa na Moi, alisema kuwa uamuzi wake wa kuingia na kuunga mkono kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi pamoja na kukubali kuachia madaraka kwa amani mwaka 2002, ni matendo mema zaidi ya kisiasa yanayopaswa kuenziwa.
“Kila mtu ana upande chanya. Wakati wowote nchi ilipokuwa inaingia kwenye hali ya joto, Moi alikuwa akirudi nyuma na kuwapa nafasi watu waongee,” alisema.
Moi aliyekuwa Rais wa pili wa Kenya, alifariki usiku wa kuamkia Februari 4, 2020 katika Hospitali ya Nairobi alikokuwa amelazwa tangu Septemba 2019. Alikuwa rais wa nchi hiyo kwa miaka 23.