Rais wa Klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Moise Katumbi ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuipokea timu yake ambayo itatumia Uwanja wa Benjamin Mkapa katika mchezo wake wa African Football League (AFL), dhidi ya Esperance Tunis ya Tunisia.
TP Mazembe na Esperance zinatarajia kupambana kesho Jumapili (Oktoba 22) katika mchezo wa Robo Fainali wa michuano ya AFL.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Katumbi amesema amefurahi kuona timu za nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADIC) ambazo ni Simba, TP Mazembe na Mamelodi Sundowns kuwepo katika michuano hiyo ya msimu huu.
Tunaishukuru Serikali ya Tanzania inayoongozwa na Rais Dk, Samia Suluhu Hassan kwa kukubali timu yetu kukubaliwa kuutumia Uwanja wa Benjamin Mkapa kwani tunajisikia tupo nyumbani.
“Tanzania ni nyumbani kwetu kwani tulishachukua wachezaji hapa Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu, tuna imani ya kuendelea kushirikiana pamoja kwa maendeleo ya soka baina yetu,” amesema.
Rais huyo wa TP Mazembe alisema michuano hiyo, imeanza msimu huu kwa mara ya kwanza na kusisitiza kuwa ana imani itakuwa na faida kubwa ikiwemo kuwatangaza wachezaji mbalimbali.
“Michuano hii imeanza kwa mara ya kwanza mwaka huu na nimefurahi kuona timu za Simba, Mazembe na Sundowns zinashiriki michuano hii na nina imani itasaidia kuwatangaza wachezaji mbalimbali na thamani yao itapanda zaidi,” amesema.