Mshambuliaji wa zamani wa Young Africans David Molinga ‘FALCAO’ amesema bado mapema kuamini kama klabu hiyo itatwaa ubingwa wa Tanzania Bara msimu huu 2021/22.
Mshambuliaji huyo ambaye kwa sasa anaitumikia Namungo FC, amefunguka suala hilo baada ya kuona asilimia kubwa ya wadau wa soka nchini wameanza kuipa nafasi Young Africans kutwaa Ubinngwa wa Tanzania Bara msimu huu 2021/22, kufuatia kuanza vizuri kwa kushinda michezo yote mitano.
Young Africans imezifunga Kagera Sugar (1-0), Geita Gold FC (1-0), KMC FC (2-0), Azam FC (2-0) na Ruvu Shooting (3-1).
Molinga amesema ni mapema sana kuzungumzia ubingwa, kwa sababu anaamini mchezo wa soka una matokeo ya ajabu sana, hivyo amesisitiza suala hilo anapaswa kuulizwa baada ya mzunguuko wa pili kufia katikati.
“Siwezi kusema Young Africans itachukua ubingwa msimu huu, unaweza kuanza ligi vizuri lakini ukamaliza vibaya na unaweza kuanza vibaya ukamaliza vizuri kwa hiyo chochote kinaweza kutokea” amesema Molinga
Baada ya kucheza michezo mitano Young Africans inaongoza msimamo wa Ligi Kuu kwa kufikisha alama 15, baada ya kushinda michezo yote, ikifuatiwa na Bingwa mtetezi Simba SC yenye alama 11, iliyoshinda michezo mitatu na kutoka sare michezo miwili, huku Namungo FC inayotumikiwa na David Milonga ‘FALCAO’ ikiwa nafasi ya 11 kwa kuwa na alama 5.