Mshambuliaji mpya wa Azam FC Mkongonai Mpiana Monzizi jana usiku alianza rasmi mazoezi na kikosi cha klabu hiyo katika uwanja wa Azam Complex Chamazi.
Monzizi alianza kujumuika na wachezaji wenzake wa Azam FC, baada ya kufaulu vipimo vya afya alivyofanyiwa jana mchana jijini Dar es salaam, ikiwa ni siku moja baada ya kuwasili nchini akitokea kwao DR Congo.
Mshambuliaji huyo alionekana mwenye furaha alipoanza mazoezi na wenzake, jamboa ambalo linatoa taswira ya kufurahishwa na mazingira ya klabu yake mpya.
Ujio wa Mozinzi umekuja kuiimarisha safu ya ushambuliaji ya timu hiyo iliyoondokewa na washambuliaji wake wawili Akono Akono aliyeuzwa Malaysia, Andrew Simchimba ametolewa mkopo Ihefu fc, huku Prince Dube akiwa na majeraha ya mkono, lakini akiwa njiani kurejea kikosini.
Mshambuliaji huyo anakua mchezaji wa kwanza kusajiliwa na Azam FC chini ya utawala wa kocha kutoka nchini Zambia George Lwandamina, ambaye ana jukumu la kurejesha makali ya ushindi ndani ya kikosi cha wanalambalamba hao wa Dar es salaam.
Azam FC iliyoanza vyema msimu huu 2020/21 kwa kushinda michezo saba mfululizo ya Ligi Kuu, imekua na matokeo mabovu kwa siku za karibuni, jambo ambalo limetoa msukumo kwa viongozi na benchi la ufundi kuanza kuboresha kikosi chao.