Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka nchini Botswana Jwaneng Galaxy Morena Ramoreboli, amekiponda kikosi cha Mabingwa wa Tanzania Bara Simba SC kwa kukiita dhaifu.
Ramoreboli ametoa kauli hiyo baada ya kikosi chake kupokea kipondo cha mabao 2-0 kutoka kwa Simba SC jana Jumapili (Oktoba 17), katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika hatua ya Kwanza uliochezwa mjini Gaborone, Botswana.
Kocha Ramoreboli amesema kikosi chake hakikua na bahati ya kushinda mchezo huo, lakini kilicheza vizuri muda wote na kwa bahati mbaya kilipoteza dhidi ya timu dhaifu.
Amesema atajiandaa ipasavyo kuelekea mchezo wa Mkondo wa pili utakaopigwa jijini Dar es salaam mwishoni mwa juma hili, ili kukiwezesha kikosi chake kuibuka na ushindi ugenini na kusonga mbele.
Katika hatua nyingine kocha huyo amemlaumu mwamuzi kwa kusema hakuchezesha kwa haki, kwani mara kadhaa aliipendelea Simba SC.
“Tumefungwa na timu dhaifu pia mwamuzi kawapendelea. Wachezaji wangu wameangushwa mara mbili kwenye box hakutupa penati pia walinzi wa Simba walizuia kwa mikono, Inaumiza sana ila tunajipanga kwa mchezo wa kwao.” amesema Morena Ramoreboli
Jwaneng Galaxy itakapokuwa Dar es salaam italazimika kusaka ushindi wa mabao matatu kwa sifuri ama zaidi, ili kujihakikishia nafasi ya kutinga hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mchezo wa Mkondo wa pili umepangwa kuchezwa Jumapili (Oktoba 24), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.