Kiungo Mkabaji wa Singida Fountain Gate, Morice Chukwu amekiri mechi itakayopigwa kesho Jumapili (Oktoba 08) wakiwa nyumbani dhidi ya Simba SC ni ngumu, lakini ametamba inafungika ikizingatiwa mchezo wenyewe unachezwa Uwanja wa Liti mjini Singida.
Timu hizo zitavaana huku kila moja ikitoka kupata ushindi kwenye mechi zilizopigwa ugenini juzi Alhamis (Oktoba 05), Simba SC ikiifumua Tanzania Prisons kwa mabao 3-1, huku Singida ikiichapa Mtibwa Sugar kwa bao 1-0, lililowekwa wavuni na Mkenya Elvis Rupia.
Akizungumzia mchezo huo unaomkutanisha na Simba SC aliyowahi kuhusishwa kujiunga nayo, Chukwu amesema katika timu zote za ndani msimu huu tangu atue nchini Wekundu hao ndio wamekuwa bora kwao akikumbushia mechi ya Ngao ya Jamii iliyopigwa Agosti 8, Mkwakwani na kuisha kwa sare kabla ya kutolewa kwa Penati 4-2.
Amesema mechi ya kesho Jumapili (Oktoba 08) inaonekana kuwa mgumu, lakini wamepania kushinda.
“Nimecheza mechi kadhaa hapa Tanzania, lakini Simba SC ndio imekuwa timu ngumu mpaka sasa. Wana timu yenye wachezaji wakubwa unatakiwa kila wakati uwe mchezoni,” amesema Chukwu aliyesajiliwa kutoka Rivers United ya Nigeria.
“Tunakwenda kucheza mechi ngumu nyingine zaidi na Simba SC lakini naamini tutafanya vizuri kwa kuwa hata sisi tumeanza kukaa sawa.”
Msimu uliopita kwenye ligi uwanjani hapo, Simba SC ililazimika kuchomoa bao la kupata sare ya 1-1.