Kocha Mkuu wa Namungo FC Hemed Morocco amesema baada ya kikosi chake kuondolewa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho (ASFC) kwa kufungwa mabao 2-0 na Biashara United Mara, hana budi kugeuzia nguvu kwenye michezo iliyosalia ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2020/21.

Namungo FC ambayo msimu uliopita ilitinga hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho na kucheza dhidi ya Mabingwa watetezi wa michuanio hiyo Simba SC jana Jumapili (Mei 23), ilishindwa kufurukuta ikiwa ugenini mjini Musoma mkoani Mara, kwenye uwanja wa Karume.

Baada ya mchezo huo Kocha Morocco alizungumza na waandishi wa habari na kueleza ameridhishwa na matokeo hayo, na anaamini uchovu wa wachezaji wake kutokana na ratiba ilikua sababu ya kukubali kupoteza.

“Tulishindwa kuzuia vizuri na jambo zuri tumefungwa mabao mawili pekee lakini ingekua hatari zaidi. Nawapongeza biashara kwa kutumia vizuri nafasi walizopata.”

“Nadhani tulitumia nguvu nyingi kwenye michuano ya kombe la shirikisho Afrika, Kwa sasa tunaangalia zaidi jinsi ya kumaliza vizuri ligi kuu na kuandaa kikosi chetu kwaajili ya msimu ujao”.  Amesema Kocha Hemed Morocco.

Katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara Namungo FC inashika nafasi ya 10 ikiwa na alama 37, baada ya kucheza michezo 27.

Namungo FC imebakiza michezo saba kumaliza msimu huu 2020/21, na itatakiwa kushinda michezo hiyo ili kujiimarisha katika nafasi za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Dangote kuineemesha Tanzania
Mashine yatumbukia baharini katika Bandari ya Dar es Salaam