Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes), Hemedi Suleiman Morocco, amesema bado hajasaini mkataba wa kuitumikia Namungo FC inayoshiriki Ligi Kuu Bara.

Kocha Morocco ambaye aliwahi kufanya kazi na klabu za Coatsl Union na Mbao FC amesema bado anaendelea na mazungumzo na viongozi wa klabu hiyo ya mkoani Lindi ambayo itashiriki michuano ya Kombe La Shirikisho Afrika (CAF).

Kikosi cha Namungo FC kimeweka kambi visiwani Zanzibar kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Young Africans utakaochezwa Jumapili pamoja na mchezo wa kwanza wa Kombe La Shirikisho Afrika dhidi ya Al Rabita FC ya Sudan Kusini.

Morocco amesema bado hajaanza kukinoa kikosi hicho, lakini mazungumzo yatakapokamilika, ataanza kazi hiyo mara moja.

Morocco ambaye pia aliwahi kuwa kocha msaidizi wa timu ya taifa ya Tanzania wakati wa utawala wa kocha kutoka nchini Nigeria Emmanuel Amunike, amesema mpira ndio kazi yake na hatasita kujiunga na klabu yoyote iwe Tanzania Bara au visiwani, endapo watafikia makubaliano.

“Tumekuwa na mazungumzo ya zaidi ya wiki mbili, kama yatakamilika na kunitangaza rasmi nitaungana nao, kwa sasa bado sijaingia mkataba nao,” amesema kocha huyo.

Namungo FC walipata nafasi ya kushiriki michuano ya Kombe La Shirikisho Afrika baada ya kuwa mshindi wa pili kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho (ASFC), wakifungwa na Simba SC katika mchezo wa fainali uliochezwa mkoani Sumbawanga mwezi Agosti.

Gwajima: Namhitaji Halima Mdee, sitamuacha (Exclusive-Video)
Hatma ya Hitimana Thiery kujilikana leo

Comments

comments