Uongozi wa Halmshauri ya Manispaa ya Morogoro unajipanga kuongeza uchumi kwa kujenga Uwanja mkubwa wa Michezo, ili kuuwezesha Mkoa huo kuwa sehemu ya mikoa itakayokuwa mwenyeji wa Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON 2027).
Tanzania, Kenya na Uganbda kwa pamoja zitakuwa mwenyeji wa Fainali za AFCON 2027, na tayari zimeanza mikakati ya maandalizi, baada ya kutangazwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’.
Akizungumza kwenye kikao cha Baraza la kawaida la madiwani, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Ally Machela amesema tayari wameshatenga kiwanja katika eneo la Kiyegea na sasa wanasubiri wadau watakaosaidiana kupatikana fedha za ujenzi katika bajeti ijayo ili kukuza mapato ya Halmashauri.
Awali Diwani wa Kata ya Mindu, Zuberi Mkalaboko alisema anampongeza Rais, Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kuhakikisha mashindano hayo yanafanyika nchini.
Alisema licha ya mikoa iliyotengwa kufanyika michuano hiyo kuwa ni Arusha na Dar es Salaam, ni vizuri Morogoro ambao ni jirani na Dar es salaam wakajenga uwanja mkubwa na wa kisasa utakaoshawishi baadhi michezo kufanyika hapo.
“Tunaweza kutumia hii fursa, kama tutakuwa na uwanja wetu wenye ubora na viwango vinavyotakiwa, tunaweza kuvishawishi vyombo husika (Serikali, TFF na CAF), kuhamisha baadhi ya michezo kwenye mkoa wetu, hii itatufanya tuupe thamani kubwa na kutangaza vivutio vyetu,” alisema Makalaboko.