Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Ghana na klabu ya Simba SC Bernard Morrison ameongeza chachu ya mpambano wa Kombe la Shiriskisho Barani Afrika dhidi ya RS Berkane ya Morocco, utakaopigwa Jumapili (Machi 11).
Simba SC itakua mwenyeji wa mchezo huo wa ‘Kundi D’, Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku ikiwa na kazi kubwa ya kusaka ushindi ambao utalipa kisasi cha kupoteza kwa kufungwa 2-0 kwenye mchezo uliopita dhidi ya RS Berkane uliounguruma Februari 27, mjini Berkane-Morocco.
Morrison ametumia ukurasa wake wa Instagram kwa kuandika ujumbe uliomlenga Kocha Mkuu wa RS Berkane Florent Ibenge ambaye aliwahi kumfundisha akiwa AS Vita ya DR Congo kabla ya kutimkia Afrika Kusini.
Katika andiko hilo Morrison amemtahadharisha Kocha Ibenge kwa kumkumbusha Uwanja wa Benjamin Mkapa ni sehemu ngumu kwa timu za kigeni kutoka salama, hivyo ajiandae.
Morrison ameandika: Kila nikikuona inanikumbusha siku ambayo ulinitoa kutoka Ghana hadi Congo DR na kuniambia utanisaidia kukua ? Mengine ni historia❤️ cha kusikitisha tu ni pale kwa Mkapa Stadium tunasahau ulichofanya. ? hakuna anayepona hapa?.
Karibu Dar Es Salaam Baba❤️
Hii ni mara ya tatu kwa Kocha Ibenge kuja Dar es salaam kwa ajili ya Michuano ya Kimataifa kwa Afrika, mara mbili zilizopita alikuwa na klabu ya AS Vita ya DR Congo, mara zote amepoteza dhidi ya Simba SC.
Mara ya kwanza ilikua msimu wa 2018/19, AS Vita ilipoteza dhidi ya Simba SC kwa kufungwa mabao 2-1, kisha msimu uliopita (2020/21) alipoteza kwa mara ya pili kwa kufungwa 4-0 kwenye Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Hadi sasa Msimamo wa Kundi D, unaonyesha kuwa RS Berkane inaongoza ikiwa na alama 06, ikifuatiwa na Simba SC yenye alama o4 sawa na USGN ya Niger huku ASEC Mimosas ya Ivory Coast ikiburuza mkia ikiwa na alama 03.