Winga Bernard Morrison ndio mchezaji pekee wa Simba aliyewateka mashabiki wakati timu hiyo iipowasili kwenye uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Julius Kambarage Nyerere jijini Dar es salaam ikitokea Kigoma.
Simba iliwasili saa 5:00 asubuhi ikitokea Kigoma ilikotwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho (ASFC) baada ya kuichapa Young Africans bao 1-0.
Wachezaji wa timu hiyo walianza kutoka ndani ya uwanja saa 5:15 wakiongozwa na Hasan Dilunga, Rally Bwalya na Said Ndemla kisha kufuatiwa na wengine.
Morrison ndio alikuwa mchezaji wa mwisho kutoka ndani na kupokewa kwa shangwe na mashabiki wengi waliofika uwanjani hapo.
Mashabiki hao waliendelea kumzunguka Morrison huku wakiimba kwa kulitaja jina lake kisha kumbeba juu juu hadi kwenye basi la Simba.
Morrison ameendelea kuwateka mashabiki wengi wa soka hapa nchini kutokana na vituko vya mara kwa mara vya mchezaji huyo.
Jana baada ya mchezo wa fainali dhidi ya Young Africans Morrison alionekana amevua bukta ya timu hiyo na kuivaa kichwani huku akibaki na nguo ya ndani tu.