Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Ghana na klabu ya Simba SC Bernard Morrison amepanga kukutana na shabiki wa klabu hiyo Michael Filbert ambaye alitembea kwa miguu kutoka Kigoma mpaka Dar es Salaam.

Michael aliwasili Jijini Dar es salaam jana baada ya kutumia siku 15, na alipokelewa na mashabiki wa Simba na kundi la Simba Ushirikiano kutoka Kigogo.

Sababu kubwa ya shabiki huyo kufanya hivyo ni kwa ajili ya kushuhudia mchezo wao dhidi ya Yanga unaotarajiwa kuchezwa Julai 3, Uwanja wa Mkapa.

Morrison amepanga kukutana na shabiki huyo kwa kueleza dhamira yake kupitia Ukurasa wa Instagram wa Mwandishi wa EATV, Zainabu Rajabu baada ya kuposti habari ya shabiki huyo kutua Bongo, Morrison aliandika:”Nahitaji kumuona yeye katika chumba cha kubadilishia nguo baada ya mchezo wa leo tafadhali.”

Simba SC leo itacheza dhidi ya Mbeya City katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.


mchezo huo umepangwa kuanza mishale ya saa moja usiku, huku Simba SC ikiendelea kuongoza msimamo wa Ligi Kuu kwa kumiliki alama 70 na wapinzani wao Mbeya City wakiwa nafasi ya 13, kwa kufikisha alama 36.

Azam FC: Namungo FC walizijua mbinu zetu
Bunge lavunja rekodi bajeti mwaka wa fedha 2021/22