Kiungo mshambuliaji wa Young Africans, Bernard Morrison, ameibuka na jipya akisema kwamba, sababu kubwa ya yeye kutoenda mazoezini ni kuhofia kupigwa na mashabiki na wachezaji wa klabu hiyo.
Mbali na hilo la kupigwa, Morrison amesema pia kitendo cha mkataba wake kumalizika, ndiyo imechochea zaidi yeye kutoungana na wenzake mazoezini hadi sasa.
Morrison ambaye Julai 12, mwaka huu katika mechi ya Nusu Fainali ya Kombe La Shirikisho Tanzania Bara (ASFC) dhidi ya Simba SC, aliondoka uwanjani mara tu alipofanyiwa mabadiliko huku timu yake ikifungwa mabao 4-1.
Tangu siku hiyo, hajaungana na wenzake hadi leo huku akisema mkataba wake umemalizika Julai 15, mwaka huu. Nyota huyo raia wa Ghana, alijiunga na Yanga, Januari mwaka huu.
Akizungumza mwishoni mwa juma lililopita, Morrison alisema: “Nimechoshwa kabisa na hali ya maisha ndani ya Yanga kwani mambo yanayoendelea kwangu na uongozi yanafanya hadi kutoelewana na nyota wenzangu.
“Nimesikia kuwa walipanga kunifanyia fujo mazoezini na ndiyo maana nikaona kwa kuwa mkataba wangu umemalizika ni bora nikae pembeni hadi pale nitakapopata muafaka wa madai yangu na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF),” alisema Morrison.
Juma lililopita Morrison alionekana akifanya mazoezi mtaani akiwa na baadhi ya vijana, na picha za video za tukio hilo zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii.