Mshambuliaji kutoka nchini Zambia Moses Phiri amesema Simba SC ina nafasi kubwa ya kutinga Hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu huu 2022/23.
Simba SC iliwafahamu wapinznai wake katika Hatua ya Makundi, Jumatatu (Desemba 12), baada ya kupangwa kwa Droo ya Hatua hiyo mjini Cairo nchini Misri.
Simba SC imepangwa Kundi C na Raja Casablanca (Morocco), Horoya AC (Guinea) na Vipes SC (Uganda).
Phiri aliyesajiliwa Simba SC amesema imekua vizuri kuwafahamu wapinzani wao katika Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, hivyo anaamini Benchi la Ufundi na Viongozi wataanza mipango ya kuiwezesha timu kufanya vizuri.
Mshambuliaji huyo amesema timu zote walizopangwa nazo kwenye Kundi C ni nzuri na zina vikosi vyenye ushindani mkubwa, lakini amesisitiza kuwa, hata Simba SC ina kikosi kizuri chenye uwezo kupamba na yoyote.
“Ndiyo ni kweli Kundi letu ni gumu lakini kwa upande wetu tuna matarajio mazuri ya kutoboa na kutinga katika hatua ya Robo Fainali ambayo ndiyo malengo ya Simba SC katika kila msimu kufika hatua hiyo na kuendelea mbele.”
“Timu ambazo zipo kwenye Kundi letu zote ni nzuri na zina malengo ya kusonga mbele, lakini hata sisi sio wanyonge katika michuano hii na tutahakikisha kuwa tunapambania timu ili tuweze kufanikiwa kufika mbali zaidi,” amesema Moses Phiri
Simba SC Itaanza Kampeni ya kusaka nafasi ya kutinga Hatua ya Robo Fainali ugenini kwa kupambana na Horoya AC kati ya Februari 10–11, Kisha itacheza nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa dhidi ya Raja Casablanca kati ya Februari 17–18.
Mchezo watatu Simba SC itacheza ugenini nchini Uganda kati ya Februari 24-25, kabla ya timu hizo kukutana tena Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam Machi 07.
Simba SC itaendelea kuwa nyumbani Uwanja wa Mkapa Dar es salaam kwa kucheza dhidi ya Horoya AC kati ya Machi 17-18 na juma moja baadae, itakwenda kumalizia hatua ya Makundi ugenini kwa kukaribishwa na Raja Casablanca kati ya Machi 31- April Mosi.