Baada ya kuifungia Simba bao la ushindi katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Singida Fountain Gate, Mshambuliaji kutoka nchini Zambia, Moses Phiri, ametamba kuwa msimu huu anataka kuvuka rekodi ya mabao aliyofunga msimu uliopita.
Phiri ambaye msimu uliopita alifunga mabao 10 katika Ligi Kuu Bara, Jumapili (Oktoba 08) alichangia ushindi wa mabao 1-2 walioupata Simba SC ugenini dhidi ya Singida Fountain Gate na kuiweka timu hiyo kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara kwa kufikisha pointi 15.
Phiri amesema: “Kwangu ni jambo zuri kuona nimefanikiwa kufunga mabao mawili mpaka sasa, nilikuwa na mwanzo mzuri msimu uliopita, lakini kwa bahati mbaya nilipata majeraha na kukosa nafasi kubwa ya kucheza.
“Msimu huu malengo yangu ni kubakikisha ninafunga mabao mengi zaidi ya msimu uliopita na ikiwezekana kushindania kiatu cha ufungaji bora.”
Kwa upande mwingine, Kocha Mkuu wa Simba SC, Roberto Oliviera ‘Robertinho’ amefurahia kumuona Phiri akicheza kwa kufuata maelekezo yake.
Kocha huyo kutoka nchini Brazil amesema: “Ninafurahia kumuona Phiri akirejea katika ubora wake taratibu, hivi sasa ameonekana kubadilika kwa kucheza akifuata maelekezo yangu ambayo ninampa kabla ya kuingia uwanjani.
“Ninataka kumuona akiendelea na mwendelezo mzuri akitokea benchi, ninataka kumuona akifunga na kutengeneza mabao kila anapoingia uwanjani.”
“Phiri ni mchezaji mzuri, lakini majeraha ndio yaliyomsababishia kiwango chake kishuke, ninaamini msimu huu atarejea katika ubora wake na kuwa tegemeo katika timu.”