Mshambuliaji kutoka nchini Zambia Moses Phiri ameahidi mazito baada ya kuipeleka Klabu ya Simba SC hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu huu 2022/23, hukua kiwa kinara wa kufumania nyavu katika kikosi cha wababe hao wa Msimbazi.

Mshambuliaji huyo aliyetua Simba SC mwanzoni mwa msimu huu akitokea Zanaco FC ya nchini kwa Zambia, alifunga bao la ushindi dhidi ya Primeiro de Agosto Jumapili (Oktoba 16), ambalo lilikamilisha safari ya Mnyama kurejea Hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

Phiri amesema kitendo cha Simba SC kufika Hatua ya Makundi kina maana kubwa kwao kama Wachezaji, Benchi la Ufundi, Viongozi na Mashabiki wote, kwani wamefikia sehemu ya malengo yao msimu huu 2022/23.

“Tumefanikiwa kuingia Hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, ni furaha kwa kila mmoja kwenye klabu ya Simba SC, hii ni sehemu ya malengo yaliyowekwa na viongozi wetu, tutahakikisha tunapambana zaidi ili kufikia pale panapokusidiwa,”

“Tumepambana sana hadi kufika hapa, haikuwa kazi rahisi kwa sababu Michezo ya Ligi ya Mabingwa ina changamoto kubwa ya ushindani kwa sababu timu ni nyingi na kila moja ilitaka kufika hapa tulipofika sisi, ilitulazimu kujitoa kwa ajili ya kila mtu anayeipenda Simba SC, tunamshukuru Mungu kwa kufanikisha hili.” amesema Phiri

Katika hatua nyingine Mshambuliaji huyo mwenye Miaka 29 amesema kitendo cha yeye kufunga mabao matano katika Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika hadi sasa tangu alipoanza kuitumikia Simba SC, ni sehemu ya malengo yake aliyojiwekea msimu huu, huku akisisitiza ataendelea kufanya hivyo kama atapata nafasi kwenye Hatua ya Makundi.

“Hili la kufunga mabao matano kwenye mechi nne, nililiweka moyoni katika malengo yangu na limetimia ingawa naamini nilikuwa na nafasi ya kufunga mengine zaidi ya hayo,”

“Mabao matano ya kwenye hatua ya awali yamepita tayari, tunakwenda kucheza mechi nyingine ngumu sita hatua ya makundi na huko nahitaji kufanya vizuri zaidi ya hatua iliyopita na hilo naamini linawezekana,”

“Kufanya vizuri kwenye nafasi yangu hakuna jambo lingine zaidi ya kufunga mabao na kama nikishindwa kufanya hivyo natakiwa kuwa msahada kwa wengine kufunga mabao”

“Haikuwa kazi rahisi kufunga hayo mabao bila ya ushirikiano kutoka kwa wachezaji wengine na naamini hilo tutakwenda nalo hadi katika hatua ya makundi pamoja na mashindano ya ndani.” amesema

Ikumbukwe Kuwa Phiri aliifungia Simba mabao matatu katika ushindi wa Jumla wa 4-0 baada ya kucheza nyumbani na ugenini dhidi ya Mabingwa wa Malawi Nyassa Big Bullet, pia akafanya hivyo dhidi ya Primeiro de Agosto ya Angola kwa kufunga mabao mawili katika ushindi wa Jumla wa 4-1.

KMC FC kuikaribisha Azam FC Uwanja wa Uhuru
Chipeta awasilisha hati za utambulisho kwa Mfalme