Usajili mzito ambao unaendelea kufanywa na mabosi wa Simba SC umemuibua Mshambuliaji wa klabu hiyo kutoka Zambia Moses Phiri ambaye ameweka wazi kuwa kikosi hicho kitakuwa moto wa kuotea mbali msimu ujao 2023/24.
Simba SC wanafanya vurugu kubwa kwenye dirisha la usajili msimu huu ambapo mpaka sasa wametoa mkono wa kwaheri “Thank You’ kwa mastaa na watendaji wao tisa, huku wakiwa wametambulisha wachezaji watatu wapya ambao ni Wacameroon, Willy Onana na Che Malone Fondoh sambamba na Muivorycoast Aubin Kramo ambao wanacheza katika nafasi za ulinzi na ushambuliaji.
Phiri ni miongoni mwa mastaa ambao walikuwa na msimu mzuri ndani ya Simba mwanzoni mwa msimu uliopita 2022/23, akifanikiwa kufunga mabao 10 kabla ya baadae kupata changamoto ya majeraha.
Kikosi hicho kinachonolewa na Kocha Mkuu, Roberto Oliveira kinatarajiwa kuondoka nchini leo Jumanne (Julai 11) kwenda kuweka kambi nchini Uturuki kwa ajili ya maandalizi ya msimu wa 2023/24.
Akizungumza jijini Dar es salaam Phiri amesema: “Kila mmoja ana shauku ya kuanza msimu mpya na kupambana kwa ajili ya kuisaidia timu kushinda mataji, tunajua msimu ujao utakuwa mgumu kutokana na kuongezeka kwa ushindani kutokana na ubora wa kila timu, lakini naamini katika ubora wa wachezaji waliopo na wale wapya tutafanya vizuri.