Mshambualiaji kutoka nchini Zambia Moses Phiri amefunguka kwa undani namna alivyoitosa Young Africans na kukubali kujiunga na Simba SC miezi kadhaa kabla ya kutoa Dar es salaam Tanzania akitokea mjini Lusaka-Zambia.
Moses Phiri alisajiliwa Simba SC mwishoni mwa msimu uliopita akitokea Zanaco FC ya nchini kwao Zambia, na aliharakisha kutua nchini kabla ya msimu kumalizika ili kukamilisha taratibu za kujiunga na Miamba hiyo ya Msimbazi.
Phiri amesema ni kweli Young Africans walikua na Mpango wa kumsajili wakati mkataba wake na Zanaco FC unaelekea ukingoni, lakini juhudi na mipango iliyofanywa na mmoja wa vigogo wa Simba SC zilikwamisha safari yake ya kutua Jangwani.
“Young Africans ilionyesha dhamira ya kunichukua na kiongozi wao alinifuata kabisa Zambia, lakini Simba SC ilimtumia mmoja wa vigogo (jina tumelihifadhi) na kunisihi nisiende Yanga wala Azam, kwani walikuwa wakinihitaji”
“Kigogo huyo aliniambia wapo tayari kunipa chochote ili nitue Msimbzi kwani walikuwa wakinihitaji mno kwa kumueleza washambuliaji wake (kipindi hicho), John Bocco, Meddie Kagere na Chriss Mugalu walichemsha licha ya msimu wa nyuma kufanya vyema. Tena wanitaka nijiunge dirisha dogo.”
“Kwa heshima iliyonipa Simba sikuona sababu ya kuhangaika na wengine, ndio maana nikaipotezea Young Africans na Azam na kuamua kutua Msimbazi.”
“Nakumbuka nilimjibu kiongozi huyo naweza kufanya kazi hiyo ya kufunga bila shida yoyote nikishirikiana na wachezaji wenzangu naimani kubwa kufanya vizuri ndani ya mzunguko wa kwanza,”
“Baada ya kufika nchini kujiunga na Simba viongozi wa juu, Salim Abdallah na Barbara Gonzalez kila mmoja kwa nafasi yake aliniambia wana imani kubwa nami na kufanya vizuri kama ilivyokuwa Zambia.”
“Basi baada ya kupatiwa kila nilichokuwa nahitaji kwenye mkataba wangu deni kubwa lilibaki kwangu kutimiza yale makubaliano yetu na viongozi hao pamoja na imani kubwa waliyoiweka kwangu.”
“Nashukuru Mungu ndani ya duru la kwanza licha ya kukosa baadhi ya mechi kwa kushirikiana na wachezaji wenzangu nimeweza kufanya lile ambalo nilikuwa naimani naenda kulitimiza.”
“Simba kuna wachezaji wengi wazuri kwa kushirikiana na wao katika duru la pili naweza kufunga zaidi ya haya mabao niliyofunga sasa kwenye ligi na nikaendelea makali hadi kwenye hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika,” amesema Moses Phiri