Mshambuliaji kutoka nchini Zambia Moses Phiri yupo kwenye hatua za mwisho kuongeza mkataba mnono wa miaka miwili, ambao utaendelea kumuweka Simba SC.
Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zimeeleza kuwa Phiri baada ya mazungumzo marefu, amekubali kuongeza mkataba na klabu hiyo licha ya kupata ofa nono kutoka klabu zingine moja ya ndani hapa nchini na zingine nje zilizoonesha nia ya kumsajili.
“Phiri katupa kipaumbele sisi ili aongeze mkataba, tumempa ofa ya mkataba wenye vipengele vinne, amevisoma, amekubaliana na sisi, lakini bado hajasaini, ila tunajua wakati muafaka ukifika atafanya hivyo,” kimesema chanzo ndani ya klabu hiyo.
Inasemekana kuwa Phiri ambaye anamaliza mkataba wake msimu huu ameonesha kuridhishwa na mazingira yaliyopo kwenye klabu hiyo, pamoja na kupata mapenzi makubwa kutoka kwa wanachama na mashabiki wa timu hiyo.
“Ana amani na ameonekana kupenda mazingira ya klabu pamoja na nchi kwa ujumla, yenye mashabiki wanaopenda sana soka, mwenyewe akiwapenda sana mashabiki wa Simba kwa jinsi wanavyompa sapoti siku zote, hata kwenye nyakati ngumu alizopitia, ikiwamo kuwa majeruhi kwa muda mrefu,” amesema mtoa taarifa hizi.
Simba SC ilimsajili Mshambuliaji huyo msimu uliopita kutoka Zanaco ya Zambia na alikuwa tegemeo upande wa upachikaji mabao akiiwezesha kutinga makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu uliopita, akifunga mabao mechi zote za hatua za mwanzo dhidi ya Nyasa Big Bullets ya Malawi na Primeiro de Agosto ya Angola, kabla ya kutolewa kwenye hatua ya Robo Fainali dhidi ya Wydad Casablaca akiwa tayari ni majeruhi.
Aliumia Desemba 21, mwaka jana kwenye mechi ya Ligi Kuu msimu uliopita Uwanja wa Kaitaba, Bukoba mkoani Kagera, timu yake ikicheza dhidi ya Kagera Sugar, mchezo ukimalizika kwa sare ya bao 1-1 na kukaa muda mrefu ambapo kwa siku za karibuni ameanza kuwa fiti baada ya kutoka majeruhi akipata nafasi ya kuingia kama mchezaji wa akiba.
Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo amesema hakuna mchezaji yeyote ambaye Simba SC itataka abaki, akaondoka.
Amesema mchezaji yeyote kama anatakiwa na klabu hiyo basi atabaki, hivyo wanachama na mashabiki wa timu hiyo wasiwe na wasiwasi kuhusu mchezaji muhimu kuondoka klabuni hapo.
“Ukiona mchezaji ameondoka Simba SC ujue ameuzwa kwenda kwenye klabu kubwa zaidi Afrika na kutuingizia pesa nyingi, au aimuhitaji hivyo imempa ruhusa akatafute maisha mengine na si vinginevyo,” amesema Ahmed.
Habari zinasema kwa Sasa klabu hiyo imeanza mchakato wa kuwaongezea mikataba wachezaji wote inaowahitaji ambao watamaliza mikataba yao mwishoni mwa msimu huu.