Mshambuliaji wa Simba SC Moses Phiri amefunguka matarajio yake kuelekea msimu ujao 2023/24 wa Ligi Kuu na Michuano ya Kimataifa, baada ya kumaliza msimu uliopita 2022/23 akiwa na mabao 10.
Phiri alishindwa kuonesha makali yake msimu uliopita baada ya kupatwa na majeraha, ambayo yalimuweka nje kwa muda mrefu, na aliporejea hakuwa na makali kama alivyoanza msimu huo.
Mshambuliaji huyo kutoka Zambia amesema natamani msimu ujao uwe wa mafanikio makubwa kwake kwa kufunga mabao mengi zaidi, ili kuisaidia klabu yake, ili ifikie mafanikio ya kutwaa mataji na kufika mbali Kimataifa.
Phiri amesema baada ya msimu wa 2022/23 kumalizika, amekuwa na mapumziko mazuri nchini kwao Zambia, na anautumia muda huo kujiweka vizuri kabla ya kurejea Tanzania, kwa ajili ya kujiandaa na msimu mpya ambao utaanza miezi miwili ijayo.
“Nilianza vizuri msimu ulioisha ambao nilitamani kufunga mabao mengi kwa kadri niwezavyo, ila kila kitu Mungu anakipanga nilipanga kupambana lakini nikaumia, hata baada ya kupona tayari wengine walikuwa wanafanya vizuri, jambo lilikuwa gumu mimi kuanza moja kwa moja kikosini,” amesema Phiri aliyesajiliwa msimu uliomalizika akitokea Zanaco na kuongeza;
“Soka ni ofisi yangu lazima nifanye kazi kwa kiwango cha juu, ndio maana najiweka fiti zaidi kuhakikisha ofisi hiyo msimu ujao inakuwa na mafanikio makubwa.”
Kabla ya kuumia aliisaidia timu hiyo kufanya vizuri kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, amesema alitamani sana msimu wake wa kwanza kuvaa medali za Ligi Kuu na kufika mbali zaidi kwenye michuano ya ‘CAF’.
“Wakati najiunga na Simba, niliwahi kusema tumekuta rekodi iliyoandikwa na wenzetu ya kunyakua mataji misimu minne mfululizo, nilitamani msimu wangu wa kwanza kucheza Tanzania na sisi kuandika ya kwetu.
“Ligi ya ndani tulimaliza nafasi ya pili, hayo yote tunayachukua kama changamoto.”