Vyombo vya Dola Wilaya ya Momba Mkoani Songwe vimeanza kuchunguza chanzo cha moto ulioteketeza vyumba 43 vikiwamo 33 vya maduka katika Mji wa Tunduma, uchunguzi huo unakuja baada ya moto ulioanza usiku wa kuamkia leo kudihibitiwa saa moja asubuhi leo.
Hadi moto unazimwa hapakuwa na taarifa za Watu kujeruhiwa, Soko la Manzese, Tunduma lina vyumba takribani 700 vya biashara na vilivyoungua ni 43 vikiwamo 10 ambavyo havitumiki huku vingine 33 vilikuwa vimejaa bidhaa mbalimbali zikiwamo simu, nguo vipuri vya magari, vito na vyakula.
DC wa Momba Fakii Lulandala pamoja na kupongeza wote walioudhibiti moto ameagiza uchunguzi wa chanzo cha moto ufanywe haraka huku RPC wa Songwe akisema atatoa taarifa baada ya uchunguzi kukamilika.