Kasi ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola inaendelea kuwavuruga maafisa anaoamini kuwa ni wazembe, ambapo leo amemfukuza kikaoni Kamishna Mkuu wa Magereza, Dkt. Juma Malewa.

Waziri Lugola amemfurusha Kamishna huyo kwa kuchelewa kufika kikaoni, akichelewa dakika moja yaani saa 5:1 badala ya saa 5:00, kinyume cha nidhamu ya jeshi.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kikaoni hapo, Waziri Lugola aliagiza kuwa itakapofika saa 5 kamili asubuhi mlango wa ukumbi ufungwe. Mlango huo ulifungwa kama alivyoagizwa, lakini ulifunguliwa saa 5 na dakika 1 ili Kamishna huyo aingie.

Waziri huyo alihoji sababu za kufungua mlango ambapo licha ya Kamishna huyo kuomba radhi, alisisitiza atoke nje ya ukumbi wa kikao hicho.

Kamishna Mkuu wa Magereza, Dkt. Juma Malewa.

Katika hatua nyingine, Waziri Lugola amemuagiza Katibu Mkuu wa wizara hiyo kumshusha cheo Mkuu wa Usalama Barabarani mkoa wa Mbeya, Leopold Fungu hadi kubaki na nyota 3.

Akiendelea kupitisha fagio katika kikao hicho cha kimkakati cha wizara, Lugola aliagiza Mkuu wa Kikosi cha Zima Moto Mkoa wa Kagera, George Mrutu ashushwe cheo.

Jana, Waziri Lugola alivunja Baraza la Taifa la Usalama Barabarani pamoja na kuahidi kuwa ataliunda upya ili kuboresha utendaji na kupunguza ajali za barabarani.

 

 

 

Afande Sele ajipanga kumng’oa Sugu Mbeya 2020
Brazil kumkosa Danilo kwenye kombe la dunia