Moto mkubwa ambao chanzo chake bado hakijajulikana leo Jumapili Machi 13, 2022 umeteketeza kiwanda cha kutengeneza magodoro kinachomilikiwa na Kampuni ya GSM kilichopo eneo la Mikocheni jijini Dar es Salaam.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Zimamoto Kinondoni, Christina Sungwa, amesema wamepokea taarifa ya tukio la moto majira ya 12 asubuhi, na kufika eneo la tukio ambapo walipata msaada kutoka zimamoto wa bandari na makampuni binasfi.
“Baada ya kupata taarifa hiyo tulifika haraka eneo la tukio, tukaomba msaada kwa wenzetu wa bandari na kampuni binafsi wanaohusika na shughuli za uzimaji moto”, amesema.
Kamanda Sunga amesema hakuna taarifa yeyote ya majeruhi na mpaka sasa bado thamani halisi ya hasara iliyopatikana bado haijajulikana.
Naye, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema moto huo umedhibitiwa na haujaleta madhara makubwa kwa binadamu.