Rais wa Shirikisho la Soka Afrika ‘CAF’ Patrice Motsepe, amesema anaamini kuwa mashindano mapya ya Ligi Soka Afrika (AFL) yanaenda kuleta chachu kwenye Soka la Afrika.
Alisema hayo Dar es salaam wakati akizindua taji la AFL, ambalo litatolewa kwa mshindi wa mashindano hayo, ambayo yalizinduliwa rasmi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es salaam, Tanzaria.
Alisema kuwa anaamini mashindano hayo yataongeza ushindani kwenye mashindano yaliyoandaliwa na CAF, lakini pia yataongeza ushindani kwenye fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON).
“Tunataka kuinua soka la Afrika na kulifanya la kuvutia na kufikia viwango vya juu, jambo ambalo ni muhimu kwa soka la Afrika kuvutia na kuwa na ushindani mkubwa.
“Msimu huu tutalkuwa na timu nane, lakini katika msimu ujao timu zitaongezeka hadi kufikia 24.”
Alisema kuwa soka la Afrika limekuwa likikua, amefurahishwa na mafanikio ya Morocco, ambao walifika nusu fainali ya Kombe la Dunia nchini Qatar, lakini kwenye ngazi ya klabu TP Mazembe iliwahi kufika fainali ya klabu bingwa ya dunia.
Alisema kuwa hii ni historia kwa Tanzania kuzindua mashindano haya makubwa barani Afrika ambayo yanaenda kufanyika kwa mara ya kwanza
“Leo (jana) nilikuwa na mazungumzo na Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu maandalizi ya mashindano ya AFCON, yalikuwa mazungumzo mazuri.
“Anataka kuona mashindano ya AFCON mwaka 2027 kuwa ya kipekee, nimefurahia kazi inayofanywa na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania, Wallace Karia kwa kazi nzuri anayoifanya,” alisema Motsepe.
Alisema anajivunia nchi ya Tanzaria hasa ilivyopiga hatua kwenye michezo kwa timu ya wakubwa, vijana na wanawake kwani alikuwa sehemu ya walioshuhudia timu ya shule ya Fountain Gate iliposhinda ubingwa Afrika Kusini.