Mshambuliaji kutoka nchini Ubelgiji na Klabu ya AS Roma, Romelu Lukaku pamoja na kiungo wa timu hiyo Nicola Zalewski walilimwa kadi nyekundi baada ya kucheza rafu mbaya kwenye mechi ya Serie A mwishoni mwa juma lililopita.
Baada ya mchezo huo Kocha Jose Mourinho aligoma kuzungumza na waandishi wa habari baada ya sare ya bao 1-1 dhidi ya Fiorentina.
Lukaku alifunga bao la kuongoza dakika ya tano ya mtanange huo, baada ya kupokea krosi kutoka kwa Paulo Dybala, kabla ya dakika 64 Zalewski alipolimwa kadi nyekundu baada ya kupewa kadi mbili za njano.
Dakika tatu za mwisho kabla ya mpira kumalizika, Lukaku alimchezea rafu mbaya Christian Kouame, na kulimwa kadi nyekundu moja kwa moja.
Roma ikalazimika kucheza na wachezaji tisa uwanjani huku ikipambana kuepuka kichapo kwenye mchezo huo kufuatia kadi hizo.
AS Roma ikafanikiwa kuambulia sare lakini ilipata pigo jingine baada Dybala na Sardar Azmoun kuumia kwenye mchezo huo.
Katika mechi hiyo Mourinho alionekana mara nyingi akitoa maelekezo wakati mechi ikiendelea, bosi huyo wa Ureno aliondoka kwa hasira bila ya kuzungumza na waandishi wa habari baada ya mechi, badala yake alikwenda kumsalimia Kocha wa Fiorentina, Vincenzo Italiano na kuwakwepa waandishi wa habari.
AS Roma inashika nafasi ya nne Serie A ikiwa na pointi 25, nyuma ya AC Milan kwa pointi nne chini ya vinara wa ligi, Inter Milan.