Aliyekuwa Kocha wa Manchester United, Jose Mourinho amesema kuwa hataki tena kukutana na mtafaruku dhidi ya watu anaofanya nao kazi, hivyo kazi yake inayofuata atafanya na watu anaowapenda.
Kocha huyo Mreno ambaye hajapata kibarua tangu alipotimuliwa na Wekundu wa Old Trafford amesema kuwa ameshapata ofa za kufanya kazi na klabu kadhaa lakini amezikataa kutokana na klabu hizo kukosa tamaa na ari ya kufanikiwa.
“Kama timu haina maono, tamaa na ari sitaenda. Nilikataa kwa sababu ninataka timu yenye kiwango cha juu na lengo la kiwango cha juu. Hicho ni kipengele cha kwanza cha mahitaji yangu,” Mourinho aliiambia Telegraph.
“Kipengele cha pili cha mahitaji yangu ni huruma na upendo. Ninataka kufanya kazi na watu ambao ninawapenda. Watu ambao nina furahara ya kufanya nao kazi, ambao nina mawazo sawa na wao,” aliongeza.
Mourinho ambaye aliondolewa Manchester Desemba mwaka jana, amewahi kuwa kocha wa timu kubwa kama Chelsea, Real Madrid na Inter Milan.
Tangu alipoiacha Manchester United, Klabu hiyo imeonesha kufanikiwa ikiwa chini ya kocha mpya wa muda Ole Gunnar Solskjaer, ikipoteza mchezo mmoja.