Meneja wa klabu ya Chelsea, Jose Mourinho amesema anahisi jambo lisilo la kawaida, baada ya klabu yake kukumbana na mwanzo mbaya zaidi wa ligi kuu katika miaka 29 iliyoshuhudia akiwa katika mabenchi ya ufundi ya klabu tofauti barani Ulaya.

Mourinho ametoa kauli hiyo baada ya kukishuhudia kikosi chake kikibamizwa mabao matatu kwa moja mwishoni mwa juma lililopita na Everton, na kufikisha idadi ya michezo mitatu waliyopoteza mpaka sasa miongoni mwa michezo mitano waliyocheza tangu ligi hiyo ilipoanza mwezi uliopita.

Wachezaji wa Jose Mourinho, hii leo watakuwa mtihani mwingine wa kuanza kampeni za kusaka ubingwa wa barani Ulaya kwa kuwakaribisha Maccabi Tel Aviv kutoka nchini Israel.

Meneja wa Chelsea Mourinho, amekutana na waandishi wa habari na kueleza maandalizi ya kikosi chake kuelekea katika mchezo huo ambapo amesisitiza kutokua na shaka, licha ya mambo kumuendelea vibaya mwanzoni mwa msimu huu.

Mourinho, amesema hali iliopo sasa katika kikosi chake hakuizoea na anaona ni jambo geni kwa kuanza vibaya msimu, tena kwa kufungwa michezo mitatu miongoni mwa michezo mitano waliyocheza katika ligi mpaka sasa.

“Nawahakikishia kuwa niko salama,” alisema. “Sina raha. Sijazoea kushindwa mara nyingi hivyo lakini sasa nazoea hali hii.”

Akaongeza: “Huwezi kunitarajia niseme kila kitu kiko shwari, na kwamba kuna nicheko na mzaha. Watu wanapokosa ufanisi wanaopigania sana, basi watavunjika moyo.

“Tunajua kwamba sisi ni – mabingwa wa Uingereza. Mashabiki huimba hilo. Hakuna anayeweza kutupokonya ufanisi tuliopata kufikia sasa au vikombe tulivyoshinda au historia yetu, unaweza kujaribu lakini huwezi kufanikiwa.

“Unapozoea kushinda kila wakati, basi unapokosa kushinda unahisi jambo lisilo la kawaida. Baadhi hukabiliana na hali hii vyema, wengine hawawezi.”

Scholes Akibeza Kikosi cha Man Utd
Arsene: Muarobaini Wa Ushambuliaji Ni Theo Walcott