Shirikisho la soka nchini Ufaransa (FFF) limethibitisha kutoa ruhusa kwa kiungo Moussa Sissoko kuondoka kwenye kambi ya timu ya taifa ya nchi hiyo, kwa ajili ya kurejea nchini England ili akamilishe mpango wa kuondoka Newcastle Utd huku klabu ya Tottenham ikitajwa kuwa kwenye mchakato wa mwisho.

Taarifa zilizochapishwa kwenye ukurasa wa kijamiii wa mtandao wa Twitter wa timu ya taifa ya Ufaransa, imethibitisha kuondoka kwa kiungo huyo kwa lengo la kuwahi muda wa usajili ambao utafikia kikomo hii leo katika bara zima ya Ulaya.

Kwa muda mrefu Sissoko amekua anahusishwa na mpango wa kutaka kuondoka St James’ Park, na taarifa hizo ziliibuka siku chache baada ya klabu ya Newcastle Utd kushuka daraja mwezi Mei mwaka huu.

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 27, aliwahi kuhusishwa na mpango wa kutaka kusajiliwa na mabingwa wa soka barani Ulaya, klabu ya Real Madrid baada ya kuonyesha uwezo mkubwa wakati wa fainali za Euro 2016 akiwa na kikosi cha Ufaransa, lakini baadae mpango huo ulififia.

Endapo atafanikiwa kuondoka St James’ Park, Sissoko atakua mchezaji wa  tano kuachana na Newcastle Utd baada ya kutanguliwa na Georginio Wijnaldum, Andros Townsend, Daryl Janmaat pamoja na Papiss Cisse.

Sissoko ameshaitumikia klabu hiyo inayoshiriki ligi daraja la kwanza nchini England (Sky Bet Championship) katika michezo 133 na kufanikiwa kufunga mabao 12 tangu aliposajiliwa mwaka 2013 akitokea Toulouse ya nchini kwao Ufaransa.

Marcos Alonso Afanyiwa Vipimo Kimya Kimya
Breaking News: Chadema watangaza kuahirisha UKUTA kwa mwezi mmoja